ZAIDI YA MAFUTA: MBADALA BORA wA KIUCHUMI

Hebu fikiria uchumi unaofanya kazi kwa kila mtu - uchumi unaoundwa na kwa manufaa ya jamii nyingi zenye ujuzi mbalimbali.

Badala ya uchumi unaotegemea mashirika ya kimataifa kuchimba faida nyingi iwezekanavyo na kutumaini kwamba makombo yatatufikia, fikiria uchumi ambao unaendeshwa na watu wa ndani. Uchumi unaoadhimisha watu, bioanuwai, urithi na mandhari asilia ya kanda. Uchumi unaotoa ajira bora na usalama wa muda mrefu, endelevu wa kifedha kwa vijana, wanaume na wanawake. Uchumi ambao hautuhitaji kuharibu mazingira, kuhatarisha wanyamapori, au kuwafukuza familia kutoka kwa mashamba wanayotegemea.

Wakati enzi ya mafuta ya visukuku inafika mwisho, ni wakati wa kufanya zaidi ya kufikiria uchumi huu wa haki na jumuishi - ni wakati wa kuanza kuujenga.

Kwa muda mrefu sana, makampuni ya kimataifa ya mafuta yametoa ahadi tupu kwa watu wa Uganda na nchi jirani za Afrika ya Kati na Mashariki. Wamezishawishi serikali na wawekezaji kumwaga fedha katika miradi ya mafuta, lakini ukweli ni kwamba thamani ya mafuta inashuka na itaendelea kushuka wakati dunia inaanza kukumbatia nishati safi inayoweza kurejeshwa na kazi zinazoambatana nayo.

Ni wakati wa kuangalia zaidi ya mafuta.

 

Tumia nguvu ya sekta mbalimbali na endelevu ambazo tayari zipo na kuwekeza katika viwanda vya siku zijazo.

Misingi dhabiti ya kiuchumi haitegemei nguzo moja - inanufaika na mkondo wa mapato mseto. Kama msemo wa zamani unavyoenda, "usiweke mayai yako yote kwenye kikapu kimoja."

Badala ya kuweka kamari juu ya makadirio yanayodorora ya sekta ya mafuta na kusubiri miaka mingi kwa faida iliyoahidiwa, tunahitaji kuunga mkono sekta ambazo tayari zinafanya kazi na kuwekeza katika tasnia endelevu, inayounda kazi ya kesho.

Kwa mfano, sekta ya utalii ya Uganda inachangia takriban 7% ya pato la taifa na inatoa zaidi ya ajira 600,000. Kinyume chake, EACOP inatarajiwa kuunda ajira 200-300 pekee za kudumu. Licha ya kuwa sekta kuu ya kiuchumi na mbunifu wa nafasi za kazi nchini Uganda, utalii mara nyingi hauzingatiwi au kupuuzwa, na takriban asilimia 0.4 tu ya bajeti ya serikali imetengewa.

Kwa kuwekeza zaidi katika utalii na uhifadhi, sekta hii inaweza kuleta manufaa makubwa zaidi ya kiuchumi kwa watu wa Afrika ya Kati na Mashariki. Lakini hii inahitaji kutunza maajabu ya asili ya kanda, wanyamapori mbalimbali na tamaduni tajiri, ambayo yote yanavutia mamilioni ya wageni katika Afrika Mashariki. Hili nalo ndilo hasa EACOP itahatarisha.

Lakini kama janga la kimataifa limetukumbusha, hata utalii hauko salama kwa mshtuko wa soko la kimataifa. Ndio maana tunahitaji uchumi mseto.

Tuchukue mfano mwingine kutoka Uganda. Sekta ya kilimo inaajiri watu wengi zaidi kuliko sekta nyingine yoyote: ni uti wa mgongo wa uchumi na nchi. Bado wakulima wadogo wanaofanya tasnia hii muhimu kufanya kazi wamepuuzwa. Msaada kwa sekta hii unachangia chini ya asilimia 3 tu ya bajeti ya serikali, lakini sekta hiyo inazalisha karibu asilimia 25 ya pato la taifa.

Kuna fursa ya kweli ya kuongeza nguvu za kiuchumi na ustahimilivu kwa kuwekeza na kusaidia kilimo kidogo endelevu - ambacho huchangia pato kubwa la sekta hiyo na, tofauti na sekta ya mafuta, huajiri wanawake na vijana wengi. Kwa kusaidia sekta ya kilimo na wafanyakazi wake kwa kuzingatia usawa na uendelevu, tunaweza kuongeza mchango wa sekta ya kiuchumi katika eneo hili, huku tukihifadhi manufaa ya kimazingira, kijamii na kiafya inayotoa kwa jamii. Sekta ya uvuvi, ambayo inasaidia mamilioni ya watu, inatoa hali kama hiyo.

Lakini EACOP inatishia uwepo wa sekta hizi zote za kijani kibichi. Takriban theluthi moja ya bomba hilo litajengwa katika Bonde la Ziwa Victoria, ambalo zaidi ya watu milioni 40 wanategemea maji na uzalishaji wao wa chakula.

 

Wekeza katika nishati safi, kazi za ndani na umeme wa bei nafuu unaokuja nao.

Viwanda endelevu kama vile nishati mbadala na usafirishaji wa umeme tayari vimeimarika vyema katika kanda, lakini kutokana na kuongezeka kwa usaidizi kutoka kwa wawekezaji wa kimataifa, sekta hiyo ina uwezo wa ajabu.

Kuendeleza uzalishaji wa nishati mbadala katika nchi kama Uganda ni fursa ya kuunda kazi bora za ndani, kuendesha maelfu ya nyumba kwa bei nafuu, na kushughulikia miradi mikubwa na njia zilizowekwa maalum za kutoa umeme kwa jamii za mbali "off-grid communities".

Sekta ya nishati safi pia ina athari njema katika usawa wa kijinsia na fursa. Wakati wanawake mara nyingi wanatengwa katika sekta ya mafuta na gesi, mipango kama Solar Sister inaonyesha jinsi nishati safi inaweza kuhimiza ujasiriamali katika sekta ndogo na kushughulikia mahitaji ya ajira ya wanawake.

Sekta ya nishati safi pia itanufaisha sekta ya kilimo, kwani upelekaji wa nishati mbadala kwa ugatuzi unaweza kuongeza mavuno na kipato kwa wakulima wadogo kwa kuboresha umwagiliaji wa maji kupitia nguvu za jua na kuwasha umeme katika shughuli nyingine za kilimo kama vile kuhifadhi na usindikaji baridi.

Aidha, uwekezaji katika sekta ya nishati safi hutengeneza idadi kubwa ya ajira za kudumu katika sekta ya viwanda. Kwa mfano, Kiira Motors, kampuni ya kutengeneza magari inayomilikiwa na serikali, itaajiri Waganda 14,000 kuzalisha mabasi 5,000 ya umeme na magari mengine kwa mwaka. Kadiri magari yanavyokuwa nafuu zaidi, mahitaji ya magari ya umeme yataongezeka tu.

Ni juu ya serikali, benki za maendeleo, wawekezaji wa kimataifa na sisi sote kuunga mkono mabadiliko ya Afrika Mashariki kuelekea uchumi wa kijani kibichi. Ni lazima tuhakikishe kuwa si nchi tajiri pekee zinazopata manufaa makubwa ya kiuchumi yatakayotokana na kuachana na nishati ya mafuta.

 

Kwa kifupi, tunahitaji kuwekeza katika maisha na biashara zinazoendeleza jamii za wenyeji katika Afrika Mashariki leo - kutoka kwa utalii hadi uvuvi. Ni lazima pia tuwafunze na kuwaunga mkono wenyeji ili kuongoza sekta endelevu na yenye mafanikio ya siku zijazo, kama vile nishati safi inayoweza kurejeshwa.

Ni muhimu kutambua kwamba ukuaji wa uchumi na maendeleo yatawezekana tu ikiwa yatasukumwa na watu wa Afrika Mashariki na sio na makampuni ya kigeni ambayo yanatafuta tu kutafuta rasilimali na kupata faida zaidi iwezekanavyo. Uwekezaji - iwe kutoka kwa vyanzo vya ndani au vya kimataifa - lazima usaidie jamii za wenyeji, sio kuzinyonya au kuzihatarisha.

Ndio maana mashirika ya kiraia ya ndani yanaongoza mapambano ya #StopEACOP, na muungano wa sekta mtambuka wa wanaharakati, waelimishaji, wasanii, wanasiasa, na viongozi wa biashara katika Afrika Mashariki unatoa wito wa kuongezeka kwa uwekezaji wa kitaifa na kimataifa katika uchumi wa kijani kibichi. Vikundi hivi vya wenyeji vinafanya kazi kwa bidii kuhamasisha jamii kote Afrika Mashariki kujiunga na juhudi zao, ikiwa ni pamoja na kupitia elimu na uhamasishaji ambao unakabiliana na masimulizi ya uharibifu yanayouzwa na maslahi ya mafuta yenye nguvu.

Hakuna kurekebisha kwa haraka. Kujenga uchumi bora, wa haki, na jumuishi zaidi ambao utanufaisha kila mtu itachukua muda, lakini tunafurahi kwamba safari imeanza.